RC ANDENGENYE AKABIDHI VITENDEA KAZI KWA MAAFISA UGANI KILIMO KIGOMA
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kufanya Mapinduzi makubwa kwenye Sekta hiyo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kufanya Kilimo chenye tija.
Mhe. Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Maafisa Ugani Kilimo Mkoa wa Kigoma na kusisitiza nyenzo hizo kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Amesema sekta hiyo ni muhimu kwa ustawi wa jamii mkoani hapa kutokana na zaidi ya Asilimia 70 ya wakazi kutegemea Kilimo kama chanzo kikuu cha Uchumi kwa ajili ya kuwawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Pamoja na mchango mkubwa wa sekta hiyo wakazi katika mkoa wa Kigoma bado wanafanya kilimo cha kujikimu, hivyo dhamira ya serikali ni kufanya mageuzi makubwa kutoka aina hiyo ya kilimo na kuingia katika mfumo wa Kilimo cha kibiashara” amesema Mhe. Andengenye.
Kupitia hafla hiyo Mkuu wa Mkoa amegawa magari mawili yaliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuratibu Shughuli za Kilimo kwa ngazi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Bihigwe pamoja na mavazi maalum ya maafisa Ugani Kilimo 179 wa ngazi ya Mkoa na Halmashauri.
Aidha Andengenye amezikumbusha Halmashauri kutekeleza maagizo ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ikiwemo Halmashauri ya Kigoma Ujiji kutenga eneo ili Wizara ya Kilimo iweze kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kuratibu shughuli za umwagiliaji nchini.
Sambamba na agizo hilo, Mhe Andengenye ameukumbusha uongozi wa halmashauri ya wilaya Kibondo kutekeleza agizo la kutenga Eneo ili serikali iweze kutekeleza mradi wa ujenzi wa Soko la kisasa la zao la Muhogo huku halmashauri ya Buhigwe ikitakiwa kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao la Tangawizi.
Aidha Mhe. Andengenye amezielekeza halmashauri zote mkoani hapa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya kimkakati ili kuwawezesha wananchi kuyafikia masoko hayo kwa urahisi na kufanya biashara za mazao ya kilimo kwa tija.