DKT. MPANGO: JAMII IONGEZE UMAKINI KATIKA MATUMIZI YA VYOMBO VYA MOTO ILI KUEPUSHA AJALI

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema jamii inapaswa kuongeza umakini na weledi katika matumizi ya vyombo vya moto barabarani ili kuepusha ajali ambazo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na makosa ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema takribani asiliamia 76 ya ajali zinasababishwa na makosa ya kibinadamu ambayo yanajumuisha uendeshaji hatari, uzembe wa madereva wa magari, uzembe wa abiria, waenda kwa miguu kutokuwa makini wanapovuka barabara, mifugo isiyochungwa na kudhibitiwa barabarani na madereva kujaribu kupita magari mengine pasipo kuzingatia sheria.

Aidha, Dkt. Mpango amelitaka Jeshi la Polisi Nchini kuendelea kuimarisha doria na ukaguzi wa kushitukiza kwa vyombo vya moto pamoja na na kukagua weledi wa madereva ili kuzuia ajali zinazojitokeza kutokana na makosa ya kibinadamu.

Ameagiza pia kudhibitiwa kwa vitendo vya rushwa barabarani pamoja na kudhibiti ajali na vihatarishi vya usalama barabarani kwa kuzuia mwendokasi kwa vyombo vya moto, kusimamia uvaaji wa kofia ngumu kwa madereva wa bodaboda, kusimamia ufungaji wa mikanda kwenye magari pamoja na kuhakikisha vyombo vya moto vinakuwa na vifaa vya kulinda watoto.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )