MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI KATIKA KUPUNGUZA TATIZO LA UDUMAVU WILAYANI KIBONDO

Na Mwajabu Hoza, Kigoma

Vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Dkt. Henry Chinyuka, Mkuu wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kibondo tatizo la udumavu lilikuwa asilimia 32 mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia juhudi za pamoja kiwango hicho kimepungua hadi kufikia asilimia 23.9 mwaka wa fedha 2023/2024.

Afisa Lishe wa Wilaya ya Kibondo Tumaini Muna anasema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kupunguza kiwango cha udumavu kwa kuwa mstari wa mbele kufuatilia hali ya lishe na kuhakikisha elimu ya lishe bora inamfikia kila mwananchi na ufuatiliaji huu umejumuisha kutoa taarifa, kuandaa vipindi vya redio, makala, na habari za matukio mbalimbali zinazohusu lishe kwa watoto na wajawazito.

Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, bajeti iliyotengwa kwa ajili ya lishe ilitumika kwa asilimia 90 katika zoezi la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora na vyombo vya habari vimeendelea kutoa taarifa na kuhamasisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya lishe, hivyo kusaidia kupunguza tatizo la udumavu ambalo limepungua hadi asilimia 23.9.

Muna anabainisha juhudi mbalimbali zimefanywa ikiwemo kuandaa vipindi vya redio na makala za matukio, kutoa elimu ya lishe katika vijiji 50 na mitaa mitano kila robo mwaka kupitia siku ya afya na lishe ya kijiji na kuandaa matibabu ya utapiamlo kupitia majiko darasa ya lishe “Wahudumu wa afya wanatembea kaya kwa kaya na kutoa elimu kuhusu lishe, kuhamasisha ufugaji wa samaki na wanyama wadogo wadogo, na kilimo cha mazao yenye viini lishe kama maharage, mahindi, na mchicha” alisema Muna.

Kupitia mradi wa VHND+, watoto wanaohudhuria siku ya afya na lishe hupimwa malaria na wanapobainika kuwa na vimelea vya malaria wanapewa matibabu. Mradi wa STRONG, kwa kushirikiana na shirika la CRS, unatoa elimu ya lishe kwa vijana rika barehe na kupima hali yao ya  lishe.

Ingawa maendeleo yanaonekana kwa jamii ,  changamoto bado zipo ambapo elimu ya duni ya katika jamii, vyakula vinavyotolewa wakati wa jiko darasa havikidhi mahitaji lakini pia idadi ndogo ya wanaume wanaohudhuria siku ya lishe ya kijiji na bajeti ya masuala ya lishe ambayo haitoshelezi mahitaji.

Kwa kushirikiana na idara mtambuka kama vile kilimo, ustawi wa jamii, na maendeleo ya jamii, mikakati ya kukabiliana na changamoto hizi inajumuisha kutoa elimu mbalimbali ya kilimo, ufugaji, uvuvi na ujasiriamali. Vikao vya tahmini ya lishe ya Wilaya kila robo mwaka vinajadili utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa lishe, na mafunzo ya vitendo yanaendelea katika jamii.

Tumaini Muna anasema mikakati ya kuboresha hali ya lishe inajumuisha kutoa elimu kwa wajawazito na akinamama wanaonyonyesha, kuendelea kutenga na kutumia fedha za lishe, upimaji wa hali ya lishe kila mwezi, na matibabu ya utapiamlo. Viongozi wa vijiji na kata wanajengewa uwezo ili kusimamia shughuli za lishe katika maeneo yao.

Saida Hassan, mkazi wa Wilaya ya Kibondo, anasema licha ya kupata elimu ya lishe bora kwa wataalamu kupitia jiko darasa, tatizo la utapiamlo linaendelea kuathiri watoto kutokana na asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo kujishughulisha na shughuli zao za kilimo.

Saida anaeleza kuwa familia nyingi zinashindwa kuzingatia lishe bora kwa watoto kutokana na wazazi kujiingiza katika shughuli za kutafuta chakula na kukosa muda wa kuwahudumua watoto, huku changamoto nyingine ikiwa ni ukosefu wa ushiriki wa wanaume katika madarasa ya elimu kuhusu lishe.

Kwa jumla, mapambano dhidi ya udumavu katika Wilaya ya Kibondo yanaendelea kuwa na mafanikio, lakini juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha kwamba kila mtoto chini ya umri wa miaka mitano anapata lishe bora inayostahili.

Vyombo vya habari vinaendelea kuwa sehemu muhimu ya jitihada hizo lakini pia serikali imeendelea kuboresha huduma za lishe kwa kuwa na mikataba mbalimbali inayohusu masuala ya lishe nchini , sambamba na hilo utekelezaji wa mpango jumuishi wa taifa wa malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto nao umekuwa chachu ya utatuzi wa changamoto za lishe katika jamii.

Kupita mpango huo ambao unashirikisha wadau , na asasi za kiraia kwa lengo la kuifikia jamii kufanya uchechemuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo Lishe ambapo kwa mkoa wa Kigoma shirika la BakAid limekuwa likishirikiana na serikali kutoa elimu kwa jamii kupitia wahuduma wa ngazi ya jamii (CHW).

 

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )