WILAYA YA UVINZA, YATOA TAKRIBANI SHILINGI MILIONI 25 KWA AJILI YA KUKAMILISHA UJENZI WA KITUO CHA AFYA

Mwajabu Hoza, Kigoma.

Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, imetoa fedha takribani milioni 25 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha Sunuka, ujenzi ambao ulikuwa umesimama kwa takribani miaka mitatu.

Hatua hii ni matokeo ya jitihada za vyombo vya habari katika kuripoti kuchelewa kukamilika kwa kituo hicho, na jinsi hali hiyo inavyoathiri upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hususan wajawazito wanaokumbana na changamoto za uzazi.

Novemba 14 , 2023 mkuu wa mkoa Kigoma alifika katika eneo hilo la ujenzi wa kituo cha afya ambapo waandishi waliripoti changamoto zilizopo kwa wananchi wakiiomba serikali kukamilisha kituo chao cha afya ili wapate huduma za afya karibu na makazi yao.

Awali mnamo mwaka 2020, wananchi wa kata ya Sunuka walijitolea na kukusanya nguvu zao za pamoja kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, kwa lengo la kupunguza adha wanazokumbana nazo, hasa wajawazito wanaohitaji rufaa kwenda kituo cha afya kilichoko Ilagala.

Hali hiyo ilifanya suala la huduma za afya kuwa la dharura kwa jamii ya Sunuka ambapo walilazimika kuvuka mto malagalasi jambo lililochangia wajawazito wanaopewa rufaa kujifungulia njiani wakielekea kupata huduma za afya.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022, serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, lakini hatua za ujenzi zilisuasua tangu kuanza kwake mei 2021  hivyo kumlazimu mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, novemba 2023 kutoa maagizo maalum kwa ajili ya kuhakikisha ujenzi huo mapema iwezekanavyo.

Hata hivyo, licha ya juhudi hizo, ujenzi uliendelea kusuasua, jambo ambalo liliwafanya wananchi wa kata ya Sunuka kuendelea kusubiri huduma za afya wanazozihitaji kwa muda mrefu ili kuokoa uhai wa mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Vyombo vya habari vilipokuwa vikiendelea kuripoti hali hiyo  viliangazia  namna ambavyo uchelewaji wa mradi huo unavyoathiri jamii hususani kwa wanawake wajawazito ambapo ripoti zilizotolewa ziliangazia masikitiko ya wananchi juu ya kukamilika kwa kituo hicho.

Jenirose Juma na wengine wanaeleza kuwa wanalazimika kusafiri kwa pikipiki kwa umbali wa kilomita 20 hadi kufika kituo cha afya cha Ilagala, kwa muda wa dakika 30 lakini pia kulazimika kuvuka mto ili kupata huduma katika kituo cha afya Ilagala.

Uchambuzi wa vyombo vya habari ulileta mwangaza juu ya changamoto za upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo, na kufanya kuwa kipaumbele kwa viongozi wa serikali na watendaji wa halmashauri.

Mwandishi wa habari aliweza kuweka shinikizo kwa wahusika kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakamilika haraka na wananchi wanaanza kupata huduma karibu na makazi yao kwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa viongozi wa halmashauri.

Kwa hatua ya hivi karibuni diwani wa kata ya Sunuka Edson Telekwa anasema  halmashauri imetoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu iliyobaki na hilo linaonyesha jinsi ambavyo vyombo vya habari vilivyokuwa na mchango mkubwa katika kusukuma mbele mradi huu.

“Nashukuru sana waandishi  kwa jitihada zao za kuendelea kuripoti changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa wajawazito ambazo zimesaidia kuibua uelewa na kuchochea hatua za haraka kutoka kwa viongozi wa serikali”alisema .

Hadi sasa jumla ya majengo manne yameshakamilika  na kuwekewa baadhi ya miundombinu ambapo kwa sasa hakuna huduma ya umeme , milango kwa baadhi ya majengo pamoja na huduma zingine muhimu.

Ni matumaini kuwa fedha zilizotolewa zitachochea kasi ya ujenzi na kuhakikisha kituo cha afya cha Sunuka kinakamilika kwa wakati, hivyo kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa kata hiyo, na kuondoa adha kubwa kwa wajawazito wanaohitaji huduma za haraka.

Kwa mujibu wa taarifa za Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Uvinza Fredy Milanzi amekiri kuchelewa kukamilika kwa kituo hicho ambapo amesema halmashauri itaendelea kutenga bajeti ili kukamilisha kituo hicho kwa maslahi ya wananchi wa kata ya Sunuka.

“ Kwa sasa ujenzi unaendelea na tutahakikisha unakamilika kwa kipindi kifupi ili wananchi waweze kupata huduma ambapo katika kipindi cha 2023/2024 tumetenga Fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu iliyobaki na ndani ya mwezi septemba tutakuwa tumekamilisha kabisa ujenzi”

Milanzi anasema hatua zilizobaki za ujenzi ni ndogo lakini mara baada ya kukamilisha ujenzi huo tutakifungua  kwa sababu baadhi ya vifaa tiba tayari vipo vimehifadhiwa kwa ajili ya kituo hicho.

Ujenzi wa kituo hicho ulijumuisha chumba cha upasuaji, wodi ya wazazi, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba ya mtumishi pamoja na jengo la kufulia lambapo hadi sasa majengo kadhaa yameshakamilika bado hatua chache za ukamilishaji wa miundombinu ya umeme, maji milango na uwekaji wa vifaa tiba na madawa.

Kata ya sunuka ina vijiji nane ambapo asilimia kubwa ya wakazi wa Vijiji hivyo wanategemea Zahanati ya Kijiji iliyopo makao makuu ya Kata na hivyo kuelemewa na idadi kubwa ya wahitaji wa huduma za afya.

Kwa mujibu wa mpango jumuishi wa taifa wa makuzi , malezi na maendeleo ya awali ya mtoto PJT – MMMAM unaotekelezwa na serikali kupitia wadau mbalimbali umeendelea kuweka nyenzo muhimu katika kuhakikisha watoto wenye umri chini ya miaka nane pamoja na wajawazito wanapata huduma bora.

Mpango huo umejikita katika vipengele vitano vya uboreshaji wa afya ya mama na mtoto katika ukuaji wake ikiwemo malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali afya bora, lishe bora pamoja na  ulinzi na usalama.

Katika hili serikali imeendelea kuboresha mazingira kwenye maeneo hayo tano kwa kushirikiana na wadau ambapo kwa upande wa afya ya mama na mtoto ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali vimeendelea kujengwa na kuboreshwa lengo ni kuendelea kuokoa Maisha yao.

 

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )