JESHI LA POLISI LAPIGA MARUFUKU MAANDAMANO YA CHADEMA
Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Chadema imepanga kufanya maandamano hayo kuishinikiza Serikali ya Tanzania kueleza hatua iliyofikia juu ya matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa kwa wananchi na makada wake.
Leo Ijumaa, Septemba 13, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime amewaeleza waandishi wa habari, Moshi mkoani Kilimanjaro kuwa maandamano hayo hayatafanyika.
Misime ametoa onyo kwa viongozi wa Chadema kuacha kuhamasisha uvunjifu wa amani na kuwa atakayekaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Ameongeza kuwa, tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekwisha agiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa matukio mbalimbali na taarifa kukabidhiwa kwake, hivyo Chadema wanapaswa kutulia ili wasiharibu uchunguzi huo.