UTUMIAJI WA KILEVI, SIGARA NA KUTOTUMIA DAWA ZA FROLIC ACIDI KWA MJAZIMTO, CHANZO CHA WATOTO KUZALIWA NA MDOMO WAZI

Na Mwajabu Hoza, Kigoma.

UTUMIAJI wa kilevi,uvutaji wa sigara na kutotumiwa kwa Dawa za Frolic Acidi  kwa mjazimto kunatajwa kuwa sababu ya baadhi ya watoto kuzaliwa na tatizo la mdomo wazi kwa jina maarufu (mdomo sungura)  licha ya tafiti za kitaalamu kutoeleza moja kwa moja chanzo halisi cha tatizo hilo.

Wataalamu wanaeleza Mdomo sungura ni hali ambayo inajitokeza wakati wa kuzaliwa mtoto ambapo kati ya watoto 700 hadi 1000 wanaozaliwa duniani mmoja huzaliwa na tatizo la mdomo wazi.

Kupatikana kwa tatizo hilo inaweza kutajwa sio hatari ukilinganisha na magonjwa mengine yaliyozoeleka kwa watoto wachanga kuzaliwa nayo lakini tatizo hilo wakati mwingine linapaswa kuchukuliwa tahadhari mara baada ya mama kupata ujauzito.

Amina Fadhili anaeleza alijifungua mtoto wake wa kwanza katika moja ya zahanati iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji na mara baada ya kujifungua wataalamu walimueleza kuwa mtoto wake anatatizo la mdomo wazi.

“Daktari alinambia nimepata mtoto mwenye mdomo wazi na aliniuliza kama nilikunywa dawa za froric Acid nikamwambia ndio lakini nilichelewa kuanza kliniki nilienda nikiwa na mimba ya miezi mitano akasema hiyo ndio sababu ya kupata mtoto mwenye mdomo wazi’’

Amina anasema daktari alimshauri kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa  Maweni ili kuonana na madaktari bingwa wa upasuaji ambao watamfanyia upasuaji mtoto wake ambapo alilazimika kufika hospitali na  kuonana na daktari bingwa wa upasuaji.

Anasema mara baada ya daktari kumtazama mtoto alitoa maelekezo ikiwemo kusubiri mpaka mtoto atimize miezi mitatu na wakati huo alikuwa na wiki kadhaa na awe na kilo tano kuendelea , ndio atafanyiwa upasuaji.

“ Nilikuwa nafanya mawasiliano na daktari bingwa wa upasuaji kila wakati na kumjulisha maendeleo ya mwanangu na baada ya kutimizi miezi minne daktari alinambia nimlete ili aweze kufanyiwa upasuaji” alisema

Anasema tangu alipofika hospitali ya rufaa Maweni na kupokelewa alipatiwa kitanda ili siku inayofuata mtoto aweze kufanyiwa upasuaji na tangu alipofika hospitalini hapo hakuna gharama zozote alizotoa hadi muda wa kufanyiwa upasuaji ulipowadia.

Edisa Robart anasema yeye mtoto wake ameshafanyiwa upasuaji wa tatizo la mdomo wazi na wanasubiri kumtoa chumba cha upasuaji mara baada ya kukamilika kwa huduma ya upasuaji.

Anasema mara baada ya kupata ujauzito alikaa nyumbani hadi mimba ilipofikisha miezi mitatu ndipo alienda kuanza kliniki na anasema alishangwazwa kusikia taarifa ya kupata mtoto mwenye mdomo wazi mara baada ya kujifungua wakati yeye alifuata maelekezo yote aliyokuwa akipewa na wataalamu.

Kwa mujibu wa daktari bingwa wa magonjwa ya kike na uzazi Godbless Nelson anasema ili mjamzito aweze kuepukana na hatari ya kupata mtoto mwenye  tatizo la mgongo wazi na mdomo wazi anapaswa kuwahi kliniki mara tu anapogundua kuwa ni mjamzito.

Anasema faida za kufika kliniki mapema ni pamoja na kuanza kupata huduma vipimo ikiwemo Maambukizi ya HIV, Maralia, Kaswende, urinalysis, Kisukari, wingi wa damu, pamoja na kundi la damu vilevile ni pamoja na kutumia dawa za kuongeza damu (Fefo) pamoja na Folic kwa ajili ya kuzuia mgogo wazi kwa mtoto.

“ Endapo atachelewa kliniki hataweza kupata huduma hizi za mwanzoni kama folic,na vipimo vingine nilivyovitaja, Folic ni muhimu sana kuanza mapema,Vilevile HIV status ni muhimu sana kujulikana mwanzoni kwa maana ukiwa unamaambukizi ukaanza dawa mapema inapunguza mambukizi kwa mtoto aliyoko tumboni na anaweze zaliwa salama” Alisema daktari bingwa Nelson

Anasema kuna uwezekano kwa mtoto akazaliwa na mgongo wazi na mdomo wazi (lip and cleft palate) kwa kuwa yanatokea kwa mama ambaye hakutumia folic kwa miezi mitatu ya mwanzo (prevent Spina bifida (mgongo wazi) na lip and cleft palate).

Kulinga na Takiwmu za WHO zinataja wazi watoto 200,000 kila mwaka wanazaliwa na matatizo ya mdomo wazi tatizo ambalo bado jamii bado haijawa na uelewa wa kutosha kwa kuzingatia elimu wanayopewa na wataalam ikiwemo kuwahi vituo vya huduma mara baada ya kupata ujauzito ili kupata watoto walio salama kiafya.

Dkt. Frank Sudai ni daktari bingwa wa upasuaji hospitali ya Rufaa Maweni Mkoani Kigoma anaeleza mdomo wazi( mdoomo Sungura) ni hali ambayo inatokana na kutofunga/ kuungana  kwa sehemu ya juu ya  mdomo (Cleft lip) ama sehemu ya ndani ya kinywa cha meno( Cleft palate) na tatizo hilo linatokea katika kipindi cha uumbaji kwa wiki ya kumi hadi ya kumi na nne tangu kuingia kwa ujauzito.

Dkt. Sudai anasema tafiti za kitaalamu bado hazielezi sababu kubwa ya chanzo cha tatizo hilo lakini kuna visababishi vya kimazingira kwa mama mjamzito (Environmental factors) ambavyo vinaweza kuongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa  na tatizo la  mdomo wazi(Mdomo Sungura).

Kuna sababu za kimazingira ambazo ni magonjwa ya kuambukiza (TORCH ) hususani Rubella , baadhi ya dawa ambazo zitatumiwa na mama mjamzito kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito zinaweza kumuathiri mtoto(Diazepam,phenytoin) kisukari wakati wa ujauzito( Diabetes Mellitus ), lishe hususani kutopata dawa za Folic acid katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo lakini pia kurithi kutoka katika familia.

Anasema kuna aina nne za mdomo wazi moja ni kuwa na mpasuko kwenye mdomo wa juu unaoathiri upande mmoja wa mdomo (Unilateral cleft lip) ,ama pande zote(Bilateral cleft lip) , kuna mpasuko wa ndani kwenye kinywa (Isolated  cleft palate) na  mchanganyiko wa magonjwa ya uso(Craniofacial anomalies).

Akizungumzia matibabu ya mdomo wazi upande wa nje wa mdomo wa juu (Cleft lip conditions) matibabu yake makubwa ni upasuaji, na yanaanzia kwa watoto wenye angalau umri wa  miezi mitatu na kuendelea pasipo ukomo wa umri , uzito kuanzia wa kilo tano na kuendelea  na wingi wa damu kuanzia 10 (Hb=10g/dl) na umri hauna ukomo wa matibabu kwa upande wa mdomo wa wazi wa juu (Cleft lip surgeries).

Ule wa ndani wa sehemu ya kinywa ( Cleft palate surgeries) anatakiwa kutibiwa akiwa na umri wa miezi tisa  na sababu nyingine zikizingatiwa za uwingi wa damu ,kilo kutokana na umri wake na jinsia yake.

Anasema matibabu hayo hayalengi watoto tu bali hata wale wenye umri mkubwa nao wanaweza kufanyiwa upasuaji huo ambapo hadi sasa kuna mtu mwenye miaka 40 ambaye amefanyiwa upasuaji huu hapa katika hospitali ya Mkoa wa Maweni Kigoma.

Aidha Dkt. Sudai anasema lengo ni kuhudumia watoto wote wenye changamoto ya tatizo la mdomo wazi( Sungura) ambapo kwa mwaka 2023 lengo lilikuwa ni kufikia Watoto 40 ambapo Wateja 33 walifanyiwa upasuaji na mwaka 2024 lengo ni kuwafikia Wateja (watoto au watu wazima) 60.

Lakini pia upasuaji huu unajumuisha pia wale waliofanyiwa zamani lakini hawakufanyiwa vizuri na wanahitaji kurudiwa tena kufanyiwa,wote pia ni wanufaika wa huduma hii.

Anasema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa  Maweni-Kigoma ikishirikiana na smiletrain tangu Julai   2022 kuweza kufanikisha huduma hii na msisitizo mkubwa ni jamii iweze kuwafikisha Watoto au watu wote wenye tatizo hilo ili waweze kupatiwa huduma za upasuaji ambao unatolewa bure bila kulipia gharama zozote.

“ Huduma hii inatolewa bure kwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni kuanzia usajili,dawa vipimo,vitanda na upasuaji ambapo kwa wale wanaotoka mbali wanarudishiwa gharama za nauli pindi wafikapo na tiketi zao’’,  Amesema Dkt. Sudai.

Kwa mujibu wa hotuba ya wizara ya afya kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha kwa mwaka 2022/2023 iliyotolewa na Ummy Mwalimu inaeleza kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, jumla ya wanawake wajawazito 1,784,809 walihudhuria Kliniki na kupatiwa huduma za Afya na kati yao, asilimia 99.7 ya  wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi ikilinganishwa na asilimia 85 mwaka 2020.

Ongezeko hilo la matumizi ya huduma za kliniki wakati wa ujauzito limetokana na kubadilika kwa mwongozo wa huduma muhimu wakati wa ujauzito kutoka mahudhurio ya kila baada ya miezi mitatu na kuwa mahudhurio ya kila mwezi pamoja na kuongezeka kwa uhamasishaji juu uhumimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki ngazi ya jamii.

Hata hivyo changamoto iliyopo ni wajawazito kuchelewa kuhudhuria klinik pale tu wapatapo ujauzito na takwimu zinaonesha kati ya wajawazito 1,784,809 ni wajawazito 656,040 sawa na asilimia 37.6 walianza kupata huduma za wajawazito chini ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito, ikilinganishwa na asilimia 36 ya kipindi kama hiki mwaka 2020.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali kupitia wizara za kisekta kwa kushirikiana na asasi za kiraia inaendelea kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo kuzinduliwa kwa mpango jumuishi wa Taifa wa Makuzi , malezi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT- MMMAM) ambao unatekelezwa kwa kipindi cha 2021/2022 – 2025/26.

Lilian Mmasi kutoka shiriki la BakAid ambalo linanatekeleza mpango huo ambao unalengo kuboresha upatikanaji wa huduma kwa Watoto wenye umri wa miaka 0 – 8 ikimaanisha kuanzia ujauzito hadi hatua za ukuaji wa mtoto.

Katika kutekeleza mpango huo wao kama shirika wameendelea kufanya uchechemuzi kwa kushirikiana na serikali lakini pia kutoa elimu kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) ambao wapo katika ngazi ya jamii wanaohusika moja kwa moja kutoa elimu katika vipengele vitano ikiwemo lishe, afya, ulinzi na usalama, uchangamshi, na elimu ya awali.

Anasema lengo lao ni kumtengenezea mtoto mazingira bora na mazuri katika zile siku 1000 kuanzia mimba hadi anapotimiza miaka miwili na baada ya hapo elimu inaendelea kutolewa ili kuhakikisha mtoto huyo anakuwa katika utimilifu wake hadi umri wa miaka nane.

Mwenyekiti wa wahudumu ngazi ya jamii (CHW)   Saimon Maige anasema kulingana na elimu waliyopatiwa ya kuhudumia jamii katika suala la afya katika maeneo yao ya mitaa wanayoongoza kwa kushirikiana na serikali bado changamoto kubwa ni jamii kutokuwa na tabia ya kuhudhuria katika vituo vya kupata huduma.

Anasema wamekuwa na utaratibu wa kupita katika makazi ya watu kubaini wajawazito , Watoto chini ya umri wa miaka mitano na wenye magnjwa mbalmbali ili kuwapatia ushauri wa kufika katika vituo vya kupatia huduma lakini pia kushauri wajawazito kujifungulia katika maeneo ya kutolea huduma za afya.

“ Changamoto tuliyonayo ni elimu tunayoitoa mara nyingi haifuatwi jambo linalosababisha kuwepo kwa matukio ya wajawazito kuchelewa kufika kliniki kupata huduma za kliniki na hivyo kujikuta wakipata changamoto mara baada ya kujifungua ama kabla ya kujifungua ”

 

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )