WAKAZI KIGOMA AHIMIZWA KUJITOKEZA NA KUJIANDIKISHA KUELEKEA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amejiandikisha katika Daftari la Mkazi la Mpigakura katika Mtaa wa Shede, kata ya Kigoma katika kituo cha Ofisi ya Mtendaji kata Kigoma na kutoa wito kwa wakazi mkoani hapa kujitokeza kujiandikisha ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.
Akizungumza mara baada ya kushiriki zoezi hilo, Mhe. Andengenye amesema ni muhimu kwa wakazi kujitokeza na kujiandikisha ili kuchagua viongozi wanaowataka ambao pia watasaidia kusimamia utejelezaji wa Shughuli za Maendekeo zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita mkoani Kigoma
Amesisitiza kuwa, uchaguzi wa Viongozi katika ngazi ya kijiji na Mtaa ndicho chanzo na Mzizi wa Demokrasia nchini, hivyo kutokujiandikisha na kushiriki kupiga kura ni kujinyima haki ya kidemokrasia na kushindwa kuchagua kiongozi wanayemtaka.
“Nitoe wito kwa wakazi mkoani hapa kujitokeza ili kupata haki hiyo ya kuchagua kiongozi na kuepuka malalamiko ya kuongozwa na kiongozi ambaye hawakumchagua, wakati kwa sasa wanayo fursa ya kufanya hivyo kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa” amesema Andengenye.