UDUMAVU WA WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA MITANO BADO NI CHANGAMOTO

Na Mwajabu Hoza , Kigoma.

LICHA  ya mkoa wa Kigoma kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula cha aina mbalimbali bado tatizo la udumavu limeendelea kuwaathiri watoto chini ya umri wa miaka mitano ambapo tafiti zinaeleza kuwa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ujiji ina asilimia  34 ya udumavu huku mkoa ukiwa na asilimia 27.1

Taarifa za awali zinaeleza mkoa wa Kigoma katika kipindi cha miaka mitatu umepunguza hali ya udumavu kutoka asilimia 42.3 hadi kufikia asilimia 27.1 ambapo hatua hiyo imeelezwa kutokana na elimu kuendelea kutolewa kwa wananchi namna bora ya matumizi ya chakula kinachozalishwa.

Tukiangazia Maisha halisi kuhusu lishe na udumavu kwa upande wa jamii Tausi Othumani ni mama mwenye watoto wawili mapacha anaeleza mara baada ya kujifungua watoto wake mmoja kati yao alibainika kuwa na changamoto ya utimilifu wa viungo vya mwili lakini pia alikuwa na uzito pungufu hali iliyochangia mume wake kumtelekezea watoto.

” Nilijifungua mapacha mmoja alikuwa wa kiume na mwengine haijulikani ni wa kiume ama wakike ana jinsia ya kiume na ya kike lakini cha ajabu hiyo ya kike ni tundu tu dogo sana lenye upana kama wa tundu la sindano na ndio anapopatia haja ndogo mwanangu anaumia sana lakini pia alizaliwa na uzito wa kilo moja na hivyo kulazimika kubaki hospitali kwa muda wa wiki mbili”

Afisa lishe Manispaa Omari Kibwana akitoa elimu kwa akinamama kuhusu lishe 

Anasema kwa sasa mtoto wake ana umri wa miaka mitatu na ana kilo sita na bado hajaweza kutembea anatambaa ambapo kwa mujibu wa taarifa za afya katika ukuaji wa mtoto akiwa na umri wa miaka mitatu kama ni wa kiume anapaswa kuwa na kilo 12 -17 na kama ni wa kike anapaswa kuwa na kilo 12-16.

Ukiachilia mbali hali ya jinsia lakini pia mtoto huyo afya yake hairidhishi ambapo mama huyo anasema alishapata elimu ya lishe kutoka kwa wataalamu wa lishe lakini kutokana na hali ngumu ya kiuchumi anashindwa kumudu kufuata maelekezo ya wataalamu kumpatia mtoto chakula cha kumjenga mwili.

Tausi anaeleza kuwa kutokana na tatizo la utapiamlo alilonalo imekuwa ngumu mtoto wake kufanyiwa upasuaji ambapo daktari alimshauri kumpatia lishe ili aweze kuwa  na afya nzuri ambayo itawezesha wataalamu kumfanyia upasuaji wa njia zake.

Mwandishi wa habari hizi alilazimika kuzungumza na afisa lishe Manispaa ya Kigoma Ujiji Omari Kibwana anaeleza kutambua hali ya kiafya ya mtoto huyo ambaye alishaanza kupatiwa huduma ya lishe.

“Natambua hali ya huyo mtoto kwa mara ya kwanza namuona alikuwa na hali mbaya sana kiafya alikuwa na ukondefu uliopitiliza tulimpatia elimu mama mzazi wa mtoto huyo na kinachoendelea kwa sasa ni kuhakikisha mama anampatia mtoto lishe ya kutosha ili aweze kurejesha afya yake ya mwili ” alisema Omari.

Anasema kutokana na hali ngumu ya kiuchumi kwa mama huyo alilazimika kutoa kiasi cha fedha ili kumuwezesha Tausi kuanzisha biashara ndogondogo ambayo itamuwezesha  kumudu gharama za upatikanaji wa mahitaji muhimu ya mtoto ikiwemo chakula.

Omari anaeleza kwa sasa inakuwa ngumu kupata huduma zingine ikiwemo kufanyiwa upasuaji na matumizi ya dawa kutokana na hali yake ya kiafya ambapo inalazimika kuendelea kusubiri baadhi ya huduma hadi hapo afya yake itakapo tengamaa.

Akizungumzia athari za udumavu anaeleza kuwa udumavu unaweza kuhama kutoka kizazi hadi kizazi kingine kwa sababu aliyedumaa atashindwa kutimiza mahitaji ya familia kwa kuwa na kipato cha chini kilichosababishwa na kuwa na uelewa mdogo uliosababishwa na udumavu.

“Kwa hali hiyo mjamzito atazaa mtoto mwenye uzito pungufu na mtoto atadumaa kwa kukosa mahitaji, hata maendeleo yake ya kiakili yatakuwa chini uelewa wa darasani utakuwa wa kiwango cha chini na akikua badae atakuwa na familia yenye udumavu” Amesema Omari

Akizungumzia magonjwa ambayo yanaweza kujitokeza wakati mtoto akiwa amekosa lishe  yenye vyakula vyenye protini kama vile Nyama, Samaki, maharage , maziwa, na mayai anaweza kupata  unyafuzi na kwashakoo .

Omari anaeleza changamoto kubwa iliyopo ni uelewa mdogo wa jamii juu ya matumizi sahihi ya vyakula ambavyo vinaujenga mwili na asilimia kubwa ya wakazi wa Kigoma wanazalisha kwa wingi lakini hawajui wanakitumia vipi hicho chakula kupata lishe bora kwa watoto na hata kwa mjamzito ili aweze kupata mtoto mwenye afya bora.

Nini kinafanyika ? Omari anasema elimu inaendelea kutolewa kwa wajawazito kuhusu lishe bora katika makundi Matano ya chakula ili kupata mlo kamili ambao utawaepusha kupata watoto wenye tatizo la udumavu ambao huanzia tumboni kwa mama.

Amewasisitiza wananchi kuhudhuria siku ya afya na lishe katika maeneo yao ya mtaa, kuhudhuria kliniki ili kupata elimu ya lishe pamoja na kushiriki katika matukio ya kitaifa ya siku za lishe.

Kwa upande wa daktari bingwa wa upasuaji wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Dkt. Frank Sudai anaeleza kuwa hakuna uwezekano wa kufanyika kwa upasuaji kutokana na kuwa na hali ya utapiamlo.

Sudai anasema kuwa kinachotakiwa kufanyika kwa hatua za kwanza ni mtoto huyo akamilishe matibabu ya utapiamlo kwa kuwa hakuna udharura wa matibabu ya upasuaji kwa sasa.

Anasema mara baada ya afya kuimarika ndipo ataonwa na daktari wa kliniki ya upasuaji kwa ajili ya uchunguzi zaidi  na kuona kama ana kidhi  vigezo vya kufanyiwa upasuaji kutokana na tatizo alilonalo.

“Maadili, taratibu na miongozo  hairuhusu kufanyika kwa upasuaji ikiwa mtu ana tatizo la utapiamlo wa aina yeyote na kuna madhara mengi kabla ya upasuaji, wakati wa upasuaji hususani yanayotokana na dawa za usingizi, ndani ya chumba cha upasuaji na hata baada” amesema  Sudai.

Ikumbukwe mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa ambayo uzalishaji wake wa chakula upo kwa kiwango kikubwa lakini pia kuna rutuba nzuri ya uzalishaji wa mazao ya nafaka pamoja na matunda.

Katika kukabiliana na hali ya udumavu Mkoani Kigoma, mkuu wa mkoa Thobias Andengenye walisaini mkataba wa nyongeza ya afua za lishe katika kipindi cha mwaka 2021/2026 na wakuu wa wilaya sita waliopo Mkoani Kigoma.

Miongoni mwa maelekezo yaliyotolewa  kwa wakuu wa wilaya ni pamoja na kila halmashauri kutenga fedha kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto ili kusaidia utekelezaji wa afua za lishe kwa mkoa wa Kigoma na kuondoa tatizo la udumavu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Katika tathmini ya utekelezaji wa afua hizo za  lishe mkoa wa Kigoma kwa mwaka 2019 /2020 utekelezaji ulikuwa kwa asilimia 94.1 na kuufanya mkoa kuwa katika nafasi ya kwanza kitaifa na kwa mwaka 2020/2021 mkoa ulishuka katika  utekelezaji kwa asilimia 87.48 na kuwa nafasi ya 19.

Kwa mujibu wa mpango Jumuishi wa Taifa wa lishe wa mwaka 2021/2022 – 2025/2026 unaeleza kuwa tatizo la udumavu kwa watoto chini ya umri wa miezi 0-59 kwa mwaka 2018 umepungua kutoka asilimia 31.8 hadi kufikia asilimia 24 ikiwa ni shabaha ya mwaka 2025/2026.

Nchini Tanzania taarifa za mpango zinaeleza kuwa katika kila watoto 10  watoto watatu wamedumaa  na ili kukabiliana na hali hiyo moja ya kipaumbele ni kuhakikisha tatizo la udumavu linapungua na kumalizika hapa nchini.

Katika kukabiliana na tatizo hilo la utapiamlo shirika BakAid limekuwa likishirikiana na serikali kutekeleza mpango jumuishi wa Taifa wa malezi , makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT – MMMAM) ambapo Lilian Mmasi anasema lengo ni kuhakikisha mtoto mwenye umri wa miaka 0-8 anakuwa katika mazingira mazuri katika ukuaji wake.

Anasema wao kama shirika wametoa elimu kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) ambao wapo katika ngazi ya jamii ambao wanahusika kutoa elimu katika vipengele vitano ikiwemo lishe, afya, ulinzi na usalama, uchangamshi, na elimu ya awali.

Anasema wao wakishirikiana na serikali kupitia mpango wa PJT -MMMAM wanalenga kumtengenezea mtoto mazingira bora na mazuri katika zile siku 1000 kuanzia mimba hadi anapotimiza miaka miwili na baada ya hapo elimu inaendelea kutolewa ili kuhakikisha mtoto huyo anakuwa katika utimilifu wake hadi umri wa miaka nane.

Tukiangazia sera ya afya ya mwaka 1990 iliyopitiwa mwaka 2007 imetoa maelekezo kwa serikali inatakiwa kuweka msisitizo katika kuboresha lishe na afya za wananchi wake. Hata hivyo, juhudi za Serikali za kuhamasisha na kuelimisha jamii umuhimu wa lishe bora bado hazijapata mafanikio ya kuridhisha. Viwango vya utapiamlo bado viko juu. “Hali hii inahitaji juhudi zaidi, ili tupunguze utapiamlo katika jamii.”

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mtandao wa maendeleo ya awali ya mtoto Tanzania TECDEN na Children in cross fire (CiC) wanatekeleza mpango jumuishi wa Taifa wa makuzi , malezi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT -MMMAM) kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 – 2025/2026 ambao umekuja na utekelezaji wa vipengele vitano ikiwemo lishe.

Mpango huo unaeleza kuwa nchini Tanzania watoto milioni tatu walio chini ya miaka mitano wamedumaa, na kiwango cha utapiamlo sugu bado kipo juu suala linalotia mashaka ikizingatiwa kuwa udumavu ni kiashirikia kimojawapo kinachosababisha watoto kutofikia hatua timilifu za ukuaji.

Kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti ya mpango huo katika malengo ya muda mrefu asilimia 76 inaongezeka katika upatikanaji wa huduma bora na zilizoratibiwa na malezi jumuishi kwa Watoto wenye umri wa miaka 0-8 na walezi wao.

Christopher Peter kutoka TECDEN anaeleza mpango huo umekuwa shirikishi katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa kushirikiana na serikali pamoja na mashirika mbalimbali katika kila mkoa , mpango huu mpaka sasa umeshafika  ngazi ya Kitaifa, Mikoa hadi katika  halmashauri ambapo jumla ya halmashauri 184 nchini zimefikiwa na mpango.

Anasema malengo ya mpango ni kuhakikisha wadau wote wa kisekta na mashirika yanayotekeleza afua mbalimbali za masuala ya PJT MMMAM yanafanya kazi kwa pamoja kwenye ngazi za halmashauri na ngazi ya jamii kwa kutekeleza shughuli mbalimbali katika maeneo Matano ya mpango ikiwemo afya, lishe, ujifunzaji wa awali, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama.

Lengo la mpango ni kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka 0-8 wanakuwa katika mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu na hadi sasa mpango huo umeelezwa kufanya vizuri katika vyanja zote za maeneo Matano ya mpango kwenye ngazi ya jamii na familia.

 

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )