RC KIGOMA AICHANGIA TSH. MIL.2 TANGANYIKA BASKETBALL TEAM
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe Thobias Andengenye amekabidhi Shilingi Mil.2 kwa ajili ya kufanikisha Maandalizi ya Timu ya Mpira wa Kikapu (Tanganyika Basketball Team) ya mkoani hapa inayotarajia kushiriki Mashindano ya Klabu Bingwa Tanzania kwa mchezo huo kuanzia Novemba 9,2024 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati akipokea kikombe cha Mashindano ya Taifa Cup ambapo Timu ya wanaume ya Mkoa wa Kigoma ya mchezo huo ilishinda kupitia Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup awamu ya Nne 2024, Mkuu huyo wa mkoa ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa Sekta ya michezo kwani sambamba na kutoa burudani imekuwa ikichangia fursa za ajira kwa vijana.
Sambamba na hilo, kiongozi huyo amewaasa wachezaji wa timu hiyo kwemda kufanya vizuri katika michezo yao ili kuzidi kuuweka mkoa wa Kigoma kwenye Ramani ya mchezo wa Mpira wa Kikapu nchini.
Upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema mkoa utaendelea kuitafutia ufadhili timu hiyo ili iweze kujiimarisha na kujiweka kimashindano.
Anastus Kabonajoro ambaye ni Katibu wa Timu hiyo ameahidi kufanya vizuri katika mashindano hayo, huku akitoa wito kwa wadau wa Mchezo huo kujitokeza kwa ajili ya kuchangia na kuiwezesha timu kufanya vizuri katika mashindano hayo na mengineyo.