TARI MKOANI KIGOMA, IMESEMA HEKARI 59560 ZA MASHAMBA YA MCHIKICHI IMEPANDWA NCHINI

Mkurugenzi wa TARI Kihinga Filson  Kagimbo (kulia) akimkabidhi miche  bora ya michikichi Makamu Mwenyekiti Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kigoma (KGPC), Jacob Ruvilo.

Happiness Tesha, Kigoma.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),kituo cha Kihinga kilichopo kilichopo mkoani Kigoma, imesema hekari 59560 za mashamba ya mchikichi sawa na miche milioni 2.9 ya mbegu bora aina ya Tenera imepandwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi miche 15 ya mbegu bora za mchikichi kwa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kigoma(KGPC), Mkurugenzi wa TARI Kihinga Filson  Kagimbo  amesema hadi kufikia sasa wameshagawa miche zaidi ya milioni 4.5 kwa wakulima katika mikoa mbalimbali nchini huku kwa mkoa wa Kigoma wametoa miche milioni 1.8.

Amesema tangu kuanza kuzalisha mbegu bora ya mchikichi aina ya Tenera bado hawajafikia malengo yao kutokana na wao kuhitaji nchi nzima iweze kupandwa michikichi hiyo angalau hekta 100,000 ambapo kwasasa zimepandwa hekari 59560 pekee.

Mkurugenzi wa TARI Kihinga Filson  Kagimbo akipanda mti wa mfano baada ya kukabidhi miche  bora ya michikichi kwa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kigoma (KGPC).

Amesema wanahitaji kupanua eneo la uzalishaji wa miche hiyo nchini kwasababu wana eneo kubwa linalofaa kwa kilimo cha mchikichi nchini ambapo ni zaidi ya hekta 500,000 lakini eneo lililopandwa michikichi nchini halijafikia hata asilimia 10 ya eneo lote linalofaa kwa kilimo cha mchikichi.

“Sisi kama Tari Kihinga tutaendelea kuwa bega kwa bega na waandishi wa habari kuhakikisha tunawasaidia kuwapa elimu na ujuzi ili kuweza kutunza miche hiyo hadi watakapoanza kuvuna” amesema Kagimbo.

Amesema wao kama taasisi wataendelea kushirikiana na Kgpc  ili kuweza kueneza elimu ya zao la mchikichi kwa wakulima wa ndani na nje ya mkoa wa Kigoma kuhamasisha uwekezaji katika kilimo hicho nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa TARI Kihinga Filson  Kagimbo akipanda mti wa mfano baada ya kukabidhi miche  bora ya michikichi kwa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kigoma (KGPC).

Ofisa Kilimo kutoka Tari Kihinga, David Msigwa amesema anashauri wakulima kutumia miche ya mbegu bora ya michikichi kutokana na kuwa na mavuno mengi ukilinganisha na mbegu ya zamani, inaanza kuvunwa ndani ya miaka miwili na nusu hadi mitatu na inatoa mafuta mengi ukilinganisha na mbegu ya kienyeji.

Naye Makamu Mwenyekiti wa KGPC, Jacob Ruvilo mbali na kuishukuru Taasisi hiyo kwa kutoa miche ya mbegu bora ya zao la mchikichi, amesema kupatikana kwa miche hiyo itasaidia kuwapa uzoefu kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa wakiandika habari za wakulima wanaolima zao hilo kwa muda mrefu.

Nae Mratibu wa KGPC, Diana Rubanguka amesema juhudi zao kama chama cha waandishi wa habari ni kuanzisha miradi mbalimbali ambapo miche hiyo ya michikichi waliyopokea ni sehemu ya miradi ambayo itainua na kukiingizia kipacho chama hicho.

“Kama Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kigoma tuna mipango mingi ya kuinuka kiuchumi ikiwemo mpango huu wa kulima michikichi na baadae tuna mpango wa kununua mashine ya kukamua mafuta ikiwa ni sehemu ya miradi yetu itakayotuingizia kipato,”amesema Rubanguka

 

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )