UONGOZI MKOANI KIGOMA WATAKIWA KUENDELEA KUSIMAMIA UJENZI WA MIRADI YA MAENDELEO
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameusisitiza Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kuendelea kusimamia kwa karibu shughuli za ujenzi wa Miradi ya Maendeleo ikiwemo mradi wa upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kigoma.
Kupitia mazungumzo yake alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Ofisini kwake Leo Januari 22, 2025, Mhe Mbarawa amemuelekeza Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa, kukamilisha majengo sambamba na kuweka vifaa vya utendaji kazi katika majengo hayo ili utakapokamilika uanze kufanya kazi mara moja.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaufungua mkoa kwa kuruhusu idadi kubwa ya ndege kutoka mataifa mbalimbali kutua kwa ajili ya kuleta abiria na bidhaa za kibiashara.
Aidha Waziri huyo amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia miradi ya Maendeleo.
Akiwa mkoani hapa Waziri Mbarawa amekagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma, ambapo kesho Januari 23, 2025 atatembelea na kukagua bandari ya Kigoma sambamba na kupokea taarifa kisha kukagua ujenzi wa reli (SGR) Tabora hadi Kigoma Km. 506.
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andwngenye ameahidi kuendelea kusimamia miradi ya Maendeleo ili kuhakikisha malengo ya serikali ya kusogeza huduma kwa wananchi yanafikiwa.