WANAJESHI WA UGANDA WAKAMATWA KENYA KWA MADAI YA DHILUMA
Wanajeshi wawili wa Uganda (UPDF) wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Port Victoria, Busia, baada ya kukamatwa na maafisa wa kikosi cha ulinzi wa pwani cha Kenya wakituhumiwa kuwahangaisha wavuvi kwenye Ziwa Victoria.
Kwa muda mrefu, wavuvi wa Kenya wamelalamikia dhuluma kutoka kwa maafisa wa Uganda, ikiwemo kuporwa nyavu na kulazimishwa kula samaki wabichi.
Tukio hilo limepokelewa kwa shangwe na wavuvi wa Kenya, ambao wanaitaka serikali yao kuanzisha mazungumzo na Uganda ili kupata suluhisho la kudumu kuhusu uvuvi kwenye Ziwa Victoria.
Hadi sasa, serikali ya Uganda haijatoa tamko lolote kuhusu kukamatwa kwa wanajeshi wake. Kamishna wa Busia, Chaunga Mwachaunga, anatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu hatma ya wanajeshi hao.
Haya yanajiri huku afisa mwingine wa UPDF akiendelea kuzuiliwa katika gereza la Korinda, Busia, kwa kumuua mvuvi wa Kenya mwaka uliopita kwenye Ziwa Victoria.
Chanzo: Bbc