WAFANYABIASHARA WADOGO KIGOMA WATAKIWA KUTUMIA VITAMBULISHO VYA UJASIRIAMALI KAMA FURSA
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dr. Rashid Chuachua amewataka wafanyabiashara ndogo ndogo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kutumia vitambulisho vya ujasiriamali kama fursa ya kutambulika na taasisi mbalimbali ikiwemo za kifedha katika kujiongezea mtaji, masoko, elimu ya Ujasiriamali, mikopo na huduma mbalimbali.
Dkt Rashid ameyasema hayo wakati akizindua zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo wadogo katika Manispaa hiyo uzinduzi uliofanyika Februari 14, 2024 katika ukumbi wa Redcross kwa kugawa vitambulisho kwa Wafanyabiashara ndogondogo Mia mbili hamsini (250).
Aidha amewataka Wajasiriamali hao kutumia fursa ya mikopo ya Halmashauri na kutumia Wataalamu waliopo kupata mafunzo na elimu mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii Ndugu. Majira Jabir amesema zoezi la utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogondogo katika Manispaa hiyo unaendelea ili kuwanufaisha Wananchi wengi zaidi.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mratibu wa Vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo Manispaa ya Kigoma Ujiji Ndugu. Theonest John Nyabenda amesema vitambulisho hivyo vitawezesha kujua idadi ya wafanyabiashara na kutoa nafasi kwa Manispaa kuwa na mpango wa kuendelea kuboresha miundombinu rafiki.