CCM YAPONGEZA UBORA WA MIRADI KIGOMA DC
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma imepongeza ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Kigoma baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo wilayani humo ikiwa ni katika kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020-2025.
Miradi iliyofikiwa na Kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa Shule mpya ya Amali katika Kijiji cha Kasange unaotekelezwa na Serikali kwa Thamani ya Shilingi Mil. 603, Ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa pamoja na matundu Sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Ukombozi kwa thamani ya Shilingi Mil.118.
Katika Kata ya Simbo, kamati hiyo imekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya ambapo shughuli zinazofanyika ni ujenzi jengo la Maabara, Chumba cha upasuaji pamoja na wodi ya Mama na mtoto kwa Thamani ya Shilingi Mil.631.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni ujenzi wa tanki la Maji katika kijiji cha Mkigo kwa thamani ya Shilingi Bil.1.6, mradi wa barabara Mwandiga-Chankere unaotekelezwa kwa Thamani ya Shilingi Mil.475 pamoja na Kituo cha kupoza Umeme Kidahwe mradi unaotekelezwa kwa Shilingi Bil. 5 ambapo umefikia umefikia Asilimia 99 na kuanza kutoa huduma.
Baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Jamal Tamim ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo huku akimsisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Rashid Chuachua kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ya CCM Mkoa, yanatekelezwa kwa wakati.
Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Chuachua ameahidi kukutana na wanaosimamia utekelezaji wa miradi yote iliyotembelewa na kamati kwa lengo la kukubaliana namna bora ya kutekeleza maagizo hayo ili miradi iliyobainika kuwa na dosari ndogondogo ifanyiwe marekebisho na ile inayotoa huduma ifikie kiwango cha ufanisi kama ilivyokusudiwa na Serikali.