MRADI WA UMEME NYAKANAZI KIDAHWE MKOANI KIGOMA WAFIKIA 99%

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Mradi wa Umeme kutoka  Nyakanazi Mkoani Kagera hadi Kidahwe Kigoma Msongo wa Kv. 220 umefikia Asilimia 99 ambapo tayari mkoa wa Kigoma umeunganishwa na kuanza kutumia Umeme huo tangu  Desemba 12, 2024.

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa Thamani ya Shilingi Bil.5 unatajwa kuongeza fursa ya matumizi ya Umeme kutoka Megawati 16.5 hadi 24 pamoja na kupunguza gharama kubwa iliyokuwa ikitumika kuendesha mitambo ya kuzalisha nishati hiyo iliyokuwa ikitumia mafuta .

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo akiwa katika ziara ya Kamati ya Siasa, Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa kwa ajili ya kukagua utekelezaji Ilani ya Uchaguzi 2020-2025, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Jamal Tamim  amesema  mradi  unafungua fursa mpya kwa wawekezaji katika Sekta ya viwanda mkoani Kigoma.

Amesema awali wawekezaji wengi waliokuwa na nia ya kuwekeza  kupitia Sekta ya viwanda walishindwa kutokana na ukosefu wa Umeme wa uhakika na toshelevu.

Upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (CCM) Mkoa wa Kigoma Emmanuel Abuya amesema kukamilika kwa mradi kunaelekea kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu ya kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa eneo muhimu la kibiashara na kiuchumi kwa ukanda wa Magharibi.

Amesema mkoa unapakana na nchi za Congo DR, Burundi na hata Zambia kupitia Ziwa Tanganyika hivyo uwepo wa viwanda katika eneo hilo utatoa fursa kwa wafanyabiashara toka nchi hizo, kufuata bidhaa mkoani Kigoma badala ya kwenda maeneo mengine, jambo litakaloimarisha uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.

Katibu  wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM, Deogratius Nsokolo ameongeza kuwa, mradi huo sio umekamilisha ndoto ya muda mrefu kwa wanakigoma ya kupata umeme wa uhakika ambapo pia  utaruhusu kuchanua kwa fursa mbalimbali za ajira kwa wakazi kutokana na uwekezaji utakaofanyika.

Akitoa Taarifa ya utekekezaji wa mradi, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa Mha. Karim Namahala amesema wigo wa mradi huo ambao umefikia Asilimia 99 ni pamoja na ujenzi wa njia tano za matoleo ya Umeme Msongo wa Kv. 33 kutoka kituo cha Kidahwe kuelekea Wilaya ya Buhigwe, Kigoma Mjini, Kasulu, Uvinza na Ilagala ili kuongeza utoshelevu wa nishati hiyo katika Maeneo hayo.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )