UJENZI WA KITUO CHA AFYA MAKERE KUPUNGUZA ADHA KWA WANANCHI KUFUATA HUDUMA MBALI
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Ujenzi wa Kituo cha Afya Makere kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma utakaogharimu kiasi cha Sh.Bil. 2.62 ni utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayotaka kupanua wigo wa huduma za afya ili wananchi wasiende mbali kuzifuata huduma hizo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum),Mhe. George Mkuchika amebainisha hayo leo wilayani humo alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ikiwa ni sehemu yake ya kurudisha kwa jamii zilizopo kwenye utekelezaji wa ujenzi wa barabaraba inayotoka eneo la Kabingo hadi Buhigwe.
“Kwahiyo magonjwa mengi mliyokuwa wakati mwingine mnakwenda kuyatafutia tiba Hospitali ya Wilaya sasa huduma hizo mtazipata hapa…lakini umati kuwa mkubwa hivi inaonyesha mnakingoja kwa hamu na niwapongeze kwa kupata kituo kama hiki ambacho kinatoa huduma zote za hospitali mpaka upasuaji utakuwa unafanyika,” amesema.
Pia,amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujianda na mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao mkataba wake umesainiwa kwa kipande cha kutoka Tabora hadi nchini Burundi kwakuwa utafungua fursa nyingi za ajira hasa kwa vijana pamoja na kuimarisha suala zima la uchumi.
Katika hatua nyingine Mkuchika ameiasa jamii kuitunza amani iliyopo kwakuwa Serikali imehakikisha imedhibiti mianya yote ya uhalifu wilayani humo ambapo hadi hivi sasa hali imekuwa shwari.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kasulu,Mbelwa Chidebwe amesema kuwa wilayani humo wanatembea vifua mbele kwakuwa vitu vyote walivyovinadi kwenye kampeni za uchaguzi uliopita tayari vimevitekeleza kwa kiasi kikubwa.
Mmoja wa waudhuriaji wa tukio hilo,Everin Reuben amempongeza Mhe. Rais kwa jitihada zake za kusogeza huduma za afya karibu pamoja na kutimiza azma yake ya kumtua mama ndoo kichwani na kumtaka Waziri Mkuchika kumfikishia salamu hizo.
Ikumbukwe pindi mradi huo utakapokamilika utahusisha jengo la utawala,kichomea taka,nyumba ya mtumishi,maabara,jengo la wazazi na upasuaji,chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na idara ya wagonjwa wa ndani.