MRADI MPYA WA MAJI WILAYANI UVINZA KUMALIZA ADHA YA UPATIKANAJI WA MAJI KWA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Wananchi waishio katika Kijiji cha Mtegowanoti na Mwangaza wameondokana na adha ya kutembea mwendo wa mita 400 kufuata maji kwa matumizi mbalimbali hasa ya majumbani.
Hayo yamedhihirika mwishoni mwa wiki baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mh. Thobias Andengenye kuzindua Mradi wa Maji safi na salama uliotekelezwa na wadau Maendeleo Wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Awali akizindua mradi huo Mh. Andengenye amethibitisha zaidi ya wakazi 9000 waishio katika vijiji hivyo kuondokana na adha ya mwendo mrefu wa kupata huduma ya maji.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani mwananchi hususani kina mama, ameleta Fedha zaidi ya bilioni Moja kupunguza kilio cha jamii katika upatikanaji wa maji safi na salama kwa mashirikiano na wadau wa Maendeleo ” alisema Mh. CGF Thobias Andengenye.
Mh.Andengenye hakusita kuwapa kongole wadau wa maendeleo Poul Due Jensen, Grundfos Foundation , shirika la Umoja wa Kimataifa kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) na kushirikiana na Water mission kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Uvinza kwa kutekeleza Mradi wa maji wa Mtegowanoti na Kijiji cha Mwangaza na kuwakumbusha wananchi walinde miundombinu ya mradi huo.
Baadhi ya wananchi wa maeneo hayo hawakuficha hisia zao baada ya uzinduzi wa mradi huo na kumuibua Aziza Kashindi ambaye alikuwa na haya
“Awali tulikuwa tunashiriki maji watumiayo Mifugo lakini Leo tuna mabomba ambayo yataondoa kero nyakati za kiangazi.” Alimaliza kusema.