RC SIRRO AZINDUA ZOEZI LA CHANJO NA UTAMBUZI MIFUGO KIGOMA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Ispekta Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Polisi Mhe. Balozi Simon Sirro amewataka wafugaji Mkoani Kigoma kushiriki zoezi la chanjo ya mifugo ili kuimarisha ubora na Thamani ya mazao ya mifugo katika soko na kuongeza uchumi wa wafugaji mkoani hapa.

Sirro ametoa wito huo alipozindua rasmi zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kimkoa lililofanyika wilayani Uvinza, ambapo kwa kuanza jumla ya ng’ombe 800 na kuku 100 wamepatiwa  chanjo.

Amesema matarajio ni kuchanja jumla ya ng’ombe 340,300 pamoja na Kuku 1,780,000 ambapo zoezi hilo litafanyika kwa siku 21 tangu kuzinduliwa kwake Siku ya Leo Julai 3, 2025.

Amesema changamoto kubwa inayosababisha wafugaji kupunguza thamani ya Soko la mazao ya Wanyama kimataifa ni pamoja na majeraha kwenye ngozi za wanyama kutokana na kupigwa pamoja na uwepo wa magonjwa yanayoathiri ubora wa nyama.

Amesema mchango wa Sekta ya mifugo kwa mkoa wa Kigoma hufikia chini ya Asilimia nne ambapo hali hiyo huchangiwa na uwepo wa magonjwa ya wanyama yanayosababisha hasara kubwa kwa wafugaji.

Sirro ameendelea kusisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 ilitenga kiasi cha Shilingi Bil. 28.1 kwa ajili ya kuanza kukabiliana na magonjwa  ya homa ya ng’ombe, Sotoka ya mbuzi na Kondoo pamoja na magonjwa matatu ya kuku ambayo ni Kideri, ndui na mafua ya Kuku.

Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa faida ya chanjo hizo ni pamoja na kusaidia kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwa watu na wanyama, kuongeza uzalishaji wa mifugo, na kuongeza mapato ya Serikali kupitia Sekta hiyo.

Aidha, Mhe. Sirro ametoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi ili kuchanja mifugo yao kwani kufanya hivyo kutachangia kwa kiasi kikubwa kutokomeza magonjwa ya mifugo katika mkoa na nchi kwa ujumla.

Kupitia zoezi hilo Serikali itachangia Shilingi 500 na mfugaji Shilingi 500 kwa ajili ya chanjo ya ng’ombe, Shilingi 300 kwa chanjo ya Kondoo na Mbuzi huku chanjo hiyo ikitolewa bure kwa wafugaji wa kuku.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )