RC KIGOMA AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UZALISHAJI SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amewataka wananchi katika mikoa ya Kigoma na Tabora kujifunza mbinu bora pamoja na kutumia Teknolojia katika uzalishaji wa Mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kupiga hatua kwenye Mapinduzi ya kiuchumi kwa kengo la kujiletea Maendeleo wao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Andengenye ametoa Wito huo alipozungumza kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Nane Nane Kanda ya Magharibi yanayohusisha Mikoa ya Kigoma na Tabora yaliyofanyika katika viwanja vya Ipuli katika Manispaa ya Tabora mkoani humo, Leo Agosti 3, 2024.

Kupitia hotuba yake Mkuu wa Mkoa amesema  wananchi wanapaswa kuwatumia wataalam wa Sekta hizo kupitia maonesho hayo na wale waliopo kwenye maeneo yao wanayoishi kwa ajili ya kupata msaada wa kitaalam katika uzalishaji.

Katika hatua nyingine, Andengenye ametoa wito kwa wakulima katika mikoa hiyo kulima mazao ya Chikichi na Alizeti ili kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kupikia na kuhakikisha soko la bidhaa hiyo linaimarika ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwanufaisha kiuchumi.

Pia Mkuu huyo wa Mkoa amewashauri wakazi wa maeneo hayo kujiandaa na ushindani katika ubora wa uzalishaji na biashara kutokana na mikoa hiyo kuendelea kufunguka hali inayosababishwa na kuimarika kwa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji.

“Ongezeni kasi, ubora na ufanisi  katika uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kukabiliana na ushindani wa kimasoko  kutokana na uwekezaji mkubwa unaotarajiwa kufanywa na wawekezaji kutoka nje ya mikoa yetu kwa sababu ya kuimarika kwa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji amesema Andengenye.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )