NZI WA KUFUNGWA WATUMIKA KAMA CHAKULA CHA MIFUGO
Happiness Tesha, Kigoma.
Denis Kamanzi ni kijana aliyehitimu Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine amejiajiri kwa kuzalisha Nzi maarufu Black soldier fly ambao anawauza kama Chakula cha mifugo.
Denis ambaye amesomea Sayansi ya Chakula, pamoja na utaalamu huo ambao anao pia ameongezea maarifa yake nchini Israel ambako alihudhuria mafunzo ya kilimo na ufugaji,anasema Nzi hao wanaprotini nyingi na hivyo kuwa chakula kizuri kwa mifugo.
Denis anasema ufugaji wa Nzi hao ni muhimu kwa sasa hasa wakati huu dunia ikiwa katika tafakuri ya kuongeza uzalishaji wa chakula,gharama kubwa za ufugaji eneo moja wapo ni chakula chenye virutubisho muhimu ili kupata mazao bora, na ndio maana akafikiria kufanya shughuli hiyo.

Kijana Denis Kamanzi akiwa katika moja ya chumba akikagua pond moja wapo ya kuzalisha nzi.
“Kwa upande wa wafugaji wao wanatumia soya,dagaana uduvi kutengeneza cahakula cha kuku ambavyo na sisi binadamu tunahitaji kwenye mwili lakini pia ni gharama kwa hali hiyo inabidi tupmbane kupunguza huu mgongano wa kugombania virutubisho baina yetu na wanyama kwa kuwa na mbadala na moja ya jawabu ni hii,”amesema Denis Mfugaji wa Nzi.
Denis anasema uzalishaji wa nzi wa aina ya Black Soldier Fly ni wa gharama ndogo na usio na kazi kubwa wala kuchukua muda mrefu, na unaanzia kwenye chumba kilichopewa jina la Love cage ambapo chumba hicho kinamuwezesha dume na jike kukutana lakini pia jike atage mayai.

Pichani ni nzi katika hatua ya tano ya ukuaji.
Amesema mayai hayo badae huhamishiwa katika eneo linaloitwa ponds kwa ajili ya kutotoleshwa na kukuza hadi watakapofika hatua ya tano ya lava,huku chakula cha wadudu hao ni mabaki ya vyakula na mbolea zinazotokana na mifugo.
Amesema ufugaji wa wadudu kwasasa ni shughuli inayokuwa kwa kasi duniani kote, lengo likiwa kupata mbadala wa vuanzo vya virutubisho vinayotokana na vyanzo vya asili baadala ya maabara.

Denis Kamanzi akiwa amesimama katika eneo linaitwa ponds, eneo ambapo anatotolesha mayai na kukuza hao nzi hadi kufikia hatua ya tano.
“Kuzalisha hawa wadudu mimi situmii madawa wala kubadilisha genetic zao huyu ni mdudu halisi, maana yake ni nini, hii industry inapoeleka tunatarajia iwe mkombozi wa idadi ya watu wote duniani kwenye upande wa chakula cha mifugo na kwenye upande ya chakula cha binadamu, na wadudu wanaofugwa wako wengi, watu wanafuga mende, kuna hawa Nzi na kuna wengine wanaitwa Crickets kama sijakosea na aina nyingi nyingine na wote wanafugika kwa wepesi,”amesema Denis.

Pichani ni nzi ambao wamekaushwa ikiwa ni hatua ya mwisho tayari kwa kuuza kama chakula cha mifugo kwa wanunuzi.
Denis anaeleza kuwa uwezo wa kuzalisha hivi sasa kwa mwezi ni takriban kilo 100 ambapo anawauzia wafugaji mbalimbali kwa sh.4,000 kwa kilo ambapo wanaenda kuchanganya na chakula kingine na kutisha mifugo yao katika mikoa inayomzunguka nchini Tanzania.