TANZANIA YAANZIMISHA MIAKA 25 BILA MWALIMU JULIUS NYERERE
Watanzania wamefanya kumbukumbu ya miaka 25 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba 1999. Siku ya Nyerere, inalenga kumuezi mwasisi huyo wa taifa la Tanzania.
Katikamaadhimisho haya, wachambuzi wa siasa wamesema kuwa viongozi wa sasa bado hawajaakisi kikamilifu misingi aliyoiweka Nyerere, hasa katika eneo la umoja, maendeleo, na ushirikiano wa kikanda.
Deus Kibamba, mchambuzi wa masuala ya siasa na mwanadiplomasia, ameweka wazi kuwa Nyerere alikuwa na uthubutu wa kufanya maamuzi magumu, ambayo ni nadra kuona leo.
“Kila mtu anakubali kwamba Mwalimu alijaribu mambo magumu, kiasi ambacho sijui utamtaja nani hivi leo ambaye ameweza kujaribu hata robo ya mambo hayo.”
Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere imefanyika kwa namna mbalimbali nchini, ikijumuisha misa maalum na makongamano ya kutafakari urithi wake. Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza maadhimisho hayo akiwa jijini Mwanza, ambapo alihudhuria misa maalum ya kumbukumbu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Fransisko Ksaveri, Nyakahoja.