TAKUKURU YATOA SEMINA KWA WATENDAJI WA KATA 19 KIGOMA UJIJI

Na Mwajabu Hoza, Kigoma

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma imefanya semina elekezi kwa watendaji wa kata 19 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ikiwa na lengo la kuwakumbusha wajibu wao katika mapambano dhidi ya rushwa.

Akizungumza katika semina hiyo, Mkuu wa dawati la elimu kwa Umma, Ibrahim Sadiki, alisisitiza umuhimu wa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa jamii, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Sadiki alisema TAKUKURU imeandaa mpango mkakati wa kuwafikia wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini na vyama vya siasa, ili kuongeza uelewa kuhusu athari za rushwa na ni muhimu kila mwananchi ajue wajibu wake katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki,akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuepuka vishawishi vyovyote vinavyoweza kuwaingiza kwenye vitendo vya rushwa.

Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 2024, TAKUKURU imefanikiwa kuwafikia wadau 34,695 kwa kuwapatia elimu ya rushwa  ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii nzima ya Kigoma kujitokeza na kutoa taarifa za viashiria vya kuwepo kwa vitendo  hivyo vya rushwa.

Watendaji wa kata akiwemo Kassim Kassim kata ya Kigoma Mjini alitoa wito kwa TAKUKURU kuongeza umakini na idadi ya watendaji mitaani, akitahadharisha kwamba rushwa imeongezeka sana hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Wakati huo huo, Ramadhani Mabruki na Stanslaus Ntatiye walisisitiza umuhimu wa mafunzo kuhusu usimamizi wa miradi ya maendeleo, ili kuondoa changamoto za miradi kujengwa chini ya kiwango.

Watendaji hao walionyesha ari kubwa ya kupambana na rushwa, wakisisitiza kuwa wanataka uchaguzi ujao uwe wa haki na uwazi. TAKUKURU inatarajia kuendelea na kampeni za elimu kwa umma, kuhakikisha kila mwananchi anakuwa sehemu ya mapambano hayo muhimu.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )