UTPC YAENDESHA MKUTANO WAKE MKUU KWA MWAKA 2024 SINGIDA
Na Mwandishi Wetu, Singida
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania UTPC leo tarehe 1 Novemba 2024 imeendesha mkutano wake mkuu wa mwaka 2024 mkoani Singida ambapo umehudhuriwa na wajumbe na wadau mbalimbali.
Wajumbe hao ni pamoja na Klabu 28 za Waandishi wa Habari zilizoenea kote nchini ambapo kila Klabu imetoa wawakilishi watatu kwa nafasi ya Mwenyekiti, Katibu na Mweka hazina; Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na Sekretarieti ya UTPC.
Wadau walioshiriki ni pamoja na taasisi washirika wa kihabari ambao ni International Media Support (IMS), The Journalists Workers Union of Tanzania (JOWUTA), Media Council of Tanzania (MCT), Idara ya Habari mkoani Singida na Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Serikali ya Zanzibar.
Wadau wengine ni pamoja na The Public Service Social Security Fund (PSSSF), Legal and Human Right Centre (LHRC), AZIAL na PAMAK.
Akizingumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania UTPC Bw. Deogratius Nsokolo amesema lengo la mkutano huo ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za utendaji kwa kipindi cha mwaka 2024 kwa kuangalia changamoto, mafanikio na kupanga mikakati zaidi ya kufanikisha kwa mwaka 2025.
Aidha amezungumzia mafanikio ya taasisi ya UTPC katika falsafa yake isemayo “UTPC from Good to Great” amesema tumepiga hatua kubwa hasa kwa upande wa kuongeza uaminifu kwa wadau wengi kuliko ilivyokuwa hapo awali, na kuwa hatua hii imechagizwa zaidi na nguvu iliyowekezwa ,utayari, ari na uthabiti wa kufanya kazi kwa ufanisi kwa Wajumbe wa Bodi, Sekretatieti na Klabu zake zote 28.
“Katika kipindi cha Januari 2023 hadi Oktoba 2024 UTPC imetengeneza historia mpya na kubwa ambayo haijapata kutokea, kwa kuwa na miradi saba (7) kutoka kwa wadau wafuatao:- AmericanBar Association (BAROLI), Thomson Reuters Foundation, International Media Support (IMS), Umoja wa Ulaya (European Union), Children in Crossfire (CiC), Irex na Ford Foundation” alisema Rais.
Mkutano Mkuu wa UTPC mwaka 2024 ni takwa la kikatiba ambapo kila mwaka huendeshwa na kuhudhuriwa na wajumbe husika ambao ni Klabu za Waandishi wa Habari.