MKOA WA KIGOMA SIO SEHEMU YA KUPATIA AJIRA NA KUHAMA: NAIBU WAZIRI SANGU
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema Kigoma sio mkoa wa kupatia cheki namba (ajira) na kisha kuhama kwa visingizio vya kuifuata familia au kwa sababu za ugonjwa.
Pia amewataka watumishi mkoani Kigoma kuachana na dhana ya kuwa mkoa huo ni wa pembezoni na hauna fursa za kiuchumi.
Naibu Waziri Sangu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ikiwa ni kliniki ya kimkakati ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao.
Amesema yeye kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene wamelazimika kuweka utaratibu wa kufanya klikini hiyo katika mikoa mbalimbali nchini baada ya kuona watumishi wengi wanalazimika kusafiri hadi Dodoma kwa ajili ya changamoto walizonazo za kiutumishi ambazo zingeweza kutatuliwa papo kwa papo na maafisa utumishi wao.
Naibu Waziri Sangu amesema kuna dhana imejengeka kuwa mikoa ya Magharibi ambayo ni Katavi, Kigoma na Rukwa ni mikoa ya adhabu kwa watumishi ambao wamepangiwa kufanya kazi katika maeneo hayo, jambo ambalo sio kweli.
‘’Kumekuwa na wimbi kubwa la watumishi wa umma mara tu baada ya kupata ajira huja kuripoti mkoani Kigoma huanza taratibu za kuomba uhamisho, jambo hili sio sawa kwani wananchi wa Kigoma nao wanahitaji huduma bora kama wananchi wa Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza”. amesisitiza Sangu
Amesema mtumishi wa umma atalazimika kuhama katika Mkoa wa Kigoma endapo atakuwa amekaa miaka mitatu na kuendelea na pia kama atakuwa amepata mtumishi mwenzake wa kubadilishana nae.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kirumbe Ng’enda amesema Kigoma inahitaji watumishi wachache lakini wenye utayari wa kufanya kazi katika mkoa huo na sio wale waliopelekwa baada ya kufanya vibaya katika mikoa mingine.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mbwilo Elisante amesema mkoa huo unakabiliwa na uhaba wa watumishi kwani wengi huhamishwa bila ya kupelekwa mbadala.