CHUO KIKUU HURIA KIMETAKIWA KUWA NA KOZI ZENYE UHITAJI KATIKA SOKO LA AJIRA

Na mwandishi wetu, Kigoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekitaka chuo Kikuu Huria kufanya utafiti wa kozi gani zenye uhitaji katika dunia ya sayansi na teknolojia ili kuweza kupata wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa  Desemba 5,2024 kwenye mahafali ya 43 ya chuo hicho ambayo kitaifa yamefanyika mjini Kigoma na wahitimu 4,307 walihitimu ngazi mbalimbali za elimu, waziri mkuu Majaliwa amesema ni muhimu chuo hicho kujitangaza kwa kutoa kozi bora zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira.

“Chuo kiongeze juhudi za kuwafikia wanafunzi wengi zaidi kwa Afrika Mashariki na Afrika yote kwa ujumla kwa kuandaa kozi zenye ubora zitakazowashawishi kujiunga na chuo hichi na kufanya utafiti ili kujua dunia inataka nini kwasasa,”amesema Waziri Mkuu

Aidha Waziri Mkuu amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia taaluma zinazotolewa vyuoni, kama fursa ya kuendeleza Taifa kiuchumi, kwa kufanya tafiti zenye tija, sambamba na kusaidia kuvumbua viwanda hasa katika sekta ya kilimo na kunufaisha watanzania wa hali ya chini.

Naye makamu mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda kimeiomba serikali kuharakisha ulipaji wa deni la Sh5.3 Bilioni kwa wafanyakazi wa chuo hicho kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 2020 hadi Juni,2022 ikiwa ni stahiki zao za kiutumishi ikiwepo posho za nyumba na madaraka.

Profesa Bisandi amesema deni hilo limekuwa changamoto kwao na kuwafanya watumishi wa chuo hicho kuwa na hali mbaya sana hasa wale wanaostaafu kutokupewa stahiki zao hivyo kuomba serikali kuingilia kati deni hilo liwezwe kulipwa.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amesema kufanyika kwa mahafali hayo mkoani humo ni sehemu ya mkakati wa serikali kufungua uchumi wa mkoa wa Kigoma na kuwa mkoa wa kimkakati kwenye maswala la uchumi na biashara.

“Nichukue nafasi ya kuwakaribisha wote ikiwemo wahitimu wa leo kuja kuwekeza katika mkoa wetu wa Kigoma,kama ambavyo mnaona tunayo mvua ya kutosha, ardhi ya kutosha na ni lango la biashara kwa upande wa Magharibi kutokana na jografia yetu ya kupakana na nchi jirani ya Burundi,Rwanda, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC),”amesema RC Andengenye

Wakizungumza mara baada ya kutukiwa baadhi ya wahitimu wamesema, elimu hiyo itawaletea tija na kuwaongezea ujuzi watakapoenda mtaani kujiajiri na kuajiriwa kwenye maeneo mbalimbali.

Daniel Mjema amesema safari ya kuitafuta ngazi hiyo ya elimu haikuwa lelemama bali ilihitaji nidhamu, kujituma na kuhakikisha mwanafunzi anajiwekea malengo ya kumaliza na kujiwekea mifumo ya kujipima kama yuko ndani ya malengo aliyojiwekea.

Naye James Lerombo,aliyehitimu Shahada ya Umahiri wa Uandishi wa Habari amesema eliu hiyo ni chachu katika kuboresha kazi zake na kwamba uwepo wa wasomi kwenye Taifa kunaleta mabadiliko chanya.

 

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )