WAHITIMU WA CHUO CHA TIA WABUNI MASHINE YA KUTOTOLEA VIFARANGA

Na Mwandishi wetu, Kigoma

Vijana kutoka Chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wamebuni mashine ya kutotolea vifaranga kwa kutumia teknolojia ya kisasa itakayopunguza changamoto kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo jirani.

Wakionesha ubunifu wao leo mjini Kigoma, katika mahafali ya 22, ya chuo hicho kwa kampasi ya Kigoma, ambapo wanafunzi zaidi 700 wa fani mbalimbali wamehitimu elimu zao, wamesema ujuzi waliopata chuoni hapo utawasaidia kwenda kujiajiri mtaani na si kutegemea kuajiriwa peke yake.

Mbunifu Abubakari Athuman amesema waliweza kubuni mashine hiyo baada ya kugundua mkoa wa Kigoma hauna teknolojia ya kutotoa vifaranga na wanatumia njia ya asili huku mashine zake zikiuzwa kwa gharama kubwa madukani.

Amesema mashine zao ni rahisi kutumia na uzalishaji wake ni ndani ya siku 18 huku mashine hizo zikitumia umeme wa Shilingi elfu 5 kwa mwezi mmoja.

Naye Ezekiel Kasika amesema wanaomba serikali iweze kuwashika mkono kwa kuwapa mitaji ili waweze kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya mkoa wa Kigoma.

Amesema kwasasa wanazo mashine tatu ambazo kila moja inapatikana kwa gharama ya Tsh.380,000 kwa trei moja huku zinazouzwa dukani ni zaidi ya Tsh. 500,000 bei ambayo kila mwananchi anaweza kuimudu hasa ukiwa mfugaji.

“Changamoto ya ukosefu wa mashine ya kutotolea vifaranga kwa mkoa wa Kigoma ndio zilizotupa msukumo wa kuja na ubunifu wa mashine ya aina hiyo na kama tutawezeshwa na serikali tutafika mbali zaidi na kubuni mashine za kutosha kutokana na uhitaji,”amesema mbunifu Kasika.

Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Rashid Chuachua amesema ni muhimu vijana wakachangamkia fursa ya kusoma elimu ya juu kwani idadi ya wanaojitokeza kwasasa bado ni ndogo hasa kwa mkoa wa Kigoma.

“Niwapongeze wahitimu wa leo lakini niwaambie pia elimu haina mwisho na ni muhimu kila mmoja kuona haja ya kujiendeleza kielimu kwa ngazi za juu tusiishie kusema hapa nilipofika panatosha hapana,”amesema Dc Chuachua.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Profesa Jehovaness Aikael amewataka wahitimu hao kwenda kutumia teknolojia kujitengenezea ajira.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )