TAJENI KERO ZENU ZA KIKODI ILI MPATIWE UFUMBUZI -RC KIGOMA
Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa ya kikao kilichowakutanisha na Tume ya Rais ya Maboresho ya kodi, kutoa changamoto zao za kikodi ili kupatiwa ufumbuzi na tume hiyo kwa lengo la kuendelea kuimarisha mifumo ya ulipaji kodi kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipozungumza wakati akifungua Kikao kilichowakutanisha wadau wa kodi mkoani hapa na Tume hiyo, ambapo mkuu huyo wa mkoa amewasisitiza wadau hao kutosita kutoa kero zao kisha kupendekeza namna bora ya ukusanyaji kodi usioathiri upande wowote.
Mwenyekiti wa tume hiyo Balozi Maimuna Tarishi amesema lengo la Tume ni kuboresha, kupokea na kushauri namna bora ya ukusanyaji na utoaji kodi ili kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya nchi kwa njia rafiki na rahisi.
Aidha, Mjumbe wa Tume hiyo Prof. Mussa Asad amesema kupitia mikutano inayowakutanisha na wadau wa kodi, wanajadili na kubaini maeneo yanayostahili kufikiwa kikodi ambayo bado hayajafikiwa, kufuatilia hali ya utatuzi wa malalamiko ya kikodi, kutambua wadau wa kodi sambamba na kutatua kero zinazohusiana na utozaji kodi.
Mkutano huo umewakutanisha wakuu wa taasisi za Umma na zile binafsi, wafanyabiashara wa ngazi zote pamoja wataalam kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mkoa wa Kigoma.