HALMASHAURI ZAONYWA KUTOKUWA TEGEMEZI KWA SERIKALI KUU

Mh. Zainabu Katimba ambaye ni Naibu Waziri wa TAMISEMI akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Kigoma.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
NAIBU Waziri wa nchii ofisi ya Raisi Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Zainabu Katimba amezitaka halmashauri za mkoa Kigoma kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hizo ili kuondokana na utegemezi mkubwa wa halmashauri kwa mapato kutoka serikali kuu.
Katimba alisema hayo akitoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri za mkoa Kigoma katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa na kubainisha kuwa bado halmashauri zinazo fursa kubwa ya kusimamia vyanzo walivyo navyo na kubuni vyanzo vipya ambavyo vitawezesha halmashauri kuwa na mapato ya kutosha.

Viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa wakiwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa na Naibu Waziri TAMISEMI
Alisema kuwa moja ya maeneo ambayo halmashauri inaweza kufanya ni kutengeneza miradi kwenda kwa wananchi ikiwemo miradi ya uzalishaja mali ambayo itasaidia kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi na hivyo kuziwezesha halmashauri kuongeza mapato kwa urahisi.
Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI alisema kuwa lazima wakurugenzi wa halmashauri wakune vichwa kubadili mitazamo yao ya kuona kuwa halmashauri zipo kwa ajili ya kutoa huduma pekee au kusimamia miradi bali kuhakikisha pia zinatengeneza namna ya kukusanya mapato ambayo yatasaidia katika utoaji huduma lakini utekelezaji wa miradi.
Akizungumzia agizo hilo la Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa wakurugenzi wa halmashauri za mkoa Kigoma, Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Hassan Rugwa alisema kuwa ni muhimu halmashauri kuzingatia agizo hilo kama moja ya majukumu yao na ndiyo maana serikali kuu imetoa fedha nyingi kwa mkoa huo kuwezesha kuwa na miradi ambayo itasaidia halmashauri kuongeza ukusanyaji mapato.

Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Hassan Rungwa akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa.
Rugwa alisema kuwa hadi sasa wakati serikali inatekeleza miradi mbalimbali halmashauri za mkoa Kigoma zimeweza kukusanya mapato kwa asilimia 75 na hivyo kukamilika kwa miradi ambayo serikali imetoa shilingi trilioni 11.5 itawezesha kuongezeka kwa mapato ya halmashauri maradufu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Uvinza alisema kuwa kwa sasa mkoa Kigoma umepiga hatua kubwa katika ukusanyaji mapato nah ii imekuja kutokana na maboresho mbalimbali na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati hivyo halmashauri zimeweza kubuni miradi ambayo imekuwa inachochea ongezeko la ukusanyaji mapato kwenye halmashauri zao.

Mwenyekiyti wa Halmashauri ya wilaya ya Uvinza Jakson Mateso akizungumza baada ya Kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Kigoma.