WAZIRI MKUCHIKA ATOA WITO JAMII KUMLINDA MTOTO WA KIKE

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum), Mhe.George Mkuchika (Mb)  ameitaka Jamii kuwalinda  watoto wa kike ili waweze kufikia malengo yao ya kielimu na kutimiza ndoto zao.

Amesema baadhi ya wazazi wanathubutu kuwaachisha watoto wa kike shule ili waweze kuolewa na kujipatia mifugo na mali nyinginezo, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria na utu.

Waziri Mkuchika ametoa wito huo alipozungumza na wakazi wa Wilaya ya Kakonko April 6, 2025 akiendelea  na ziara yake ya kukagua utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)2020-2025 mkoani hapa na kusisitiza kuwa, wanawake wanamchango mkubwa katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifani.

“Leo tuna Rais ambaye ni Mama yetu na tunashuhudia anavyofanya kazi kwa upendo, ujasiri na uthubutu mkubwa, hili ni jambo kubwa na liwe mfano miongoni mwetu kama wazazi na walezi” amesema Mkuchika.

Amesisitiza kuwa, wazazi wanapaswa kutambua watoto wote wanahaki sawa na iwapo watalelewa kwa kuzingatia misingi bora ya malezi basi watayafikia malengo yao ikiwemo kuishi maisha bora na kutoa michango sawa katika jamii.

Aidha Waziri Mkuchika amesema hali ya utekelezaji miradi ya maendeleo kwenye mkoa wa Kigoma inaridhisha baada ya kukagua miradi mikubwa ya ujenzi na uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu, Afya, Maji, uchukuzi na usafirishaji nchi kavu, angani na ile ya kwenye njia za Maji.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuchika, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema serikali ya mkoa itaendelea kusimamia kwa ukaribu miradi yote ya maendeleo ambapo zaidi ya Shilingi Tril.11 zimeelekezwa mkoani hapa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )