MFUMO WA SQAS KUBORESHA UTENDAJI KAZI MASHULENI
Na Mwandishi Wetu, Kasulu Kigoma
Mfumo wa Kidigitali wa Uthibiti Ubora (SQAS) utaboresha utendaji kazi mashuleni kutokana matumizi yake kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati.
Kaimu Afisa Uthibiti Ubora wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,Clement Mahanga ameyabainisha hayo leo wakati wa mafunzo ya mfumo huo kwa wathibiti ubora wa ndani ya shule na wakuu wa shule za sekondari yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kagoma makao makuu ya halmsahuri.
Amesema mafunzo hayo yanatoa fursa kwa shule zetu kujiweka katika viwango halisi vya hali iliyopo,hivyo kuimarisha utoaji wa taarifa kati ya shule na Ofisi ya Uthibiti Ubora.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,Iyogo Isuja ameongeza kuwa mfumo huu utachangia katika kuongeza uwajibikaji na kufanya tathimini kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
“Hii ni hatua muhimu katika kuboresha elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia,”amesema.
Mmoja wa washiriki wamafunzo hayo,Gumbo John,amesema kuwa tathimini za kidigitali zitasaidia kuleta mabadiliko chanya kwenye usimamizi wa elimu na kutoa wito wa utumiaji wa mfumo huo kwa ufanisi ili kufikia malengo ya halmashauri ya kutoa elimu iliyo bora.